Historia ya Mfuko

Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) ulianzishwa awali chini ya Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 12 ya mwaka 2009 kwa jina la Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji wa Maji, ukiwa na jukumu la kutoa msaada wa uwekezaji katika miradi ya huduma za maji na usafi wa mazingira pamoja na uhifadhi wa maeneo ya vyanzo vya maji (catchment areas) yanayotumika kwa uchotaji wa maji kwa ajili ya huduma ya maji. Utekelezaji halisi wa shughuli za Mfuko wa Taifa wa Maji ulianza katika mwaka wa fedha 2015/2016.

Kwa sasa, uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Maji unaongozwa na Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 05 ya mwaka 2019, ambayo inaipa Mfuko mamlaka ya kukusanya rasilimali na kutoa msaada wa uwekezaji kwa ajili ya utoaji wa huduma za maji na usimamizi wa maeneo ya vyanzo vya maji yanayotumika kwa uchotaji wa maji. Sheria hiyo pamoja na Kanuni za Mfuko wa Taifa wa Maji, Tangazo la Serikali Na. 981 la mwaka 2019, zinatoa msingi wa kisheria kwa Mfuko wa Taifa wa Maji kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.

Aidha, Miongozo ya Ufadhili wa Miradi ya Maji imeandaliwa ili kutoa maelezo ya kina zaidi, hususan kuhusu vigezo vya kuchagua miradi ya maji inayostahili kufadhiliwa.