Vyanzo vya Mapato na Matumizi
Vyanzo na Matumizi ya Mfuko
1.1 Vyanzo vya Fedha
Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, vyanzo vya fedha vya Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) ni pamoja na:
-
Fedha zitakazotengwa na Bunge kwa madhumuni ya Mfuko;
-
Fedha zitakazopokelewa kutokana na michango, misaada na mirathi kutoka chanzo chochote;
-
Vyanzo vingine vya fedha baada ya mashauriano kati ya Waziri na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha; na
-
Fedha nyingine zozote zitakazolipwa kwa Mfuko kwa mujibu wa au chini ya Sheria yoyote.
1.2 Madirisha ya Ufadhili
Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, Mfuko wa Taifa wa Maji unatakiwa kusaidia uwekezaji katika miradi ya maji kwa njia ya ruzuku au mikopo.
1.3 Ruzuku
Miradi ya maji inayostahili kufadhiliwa na Mfuko itachaguliwa kwa kuzingatia vigezo vilivyobainishwa chini ya Miongozo hii.
1.4 Mikopo
Mikopo ya Mfuko wa Taifa wa Maji yenye masharti nafuu inapatikana kwa mamlaka za maji na mashirika ya kijamii kwa ajili ya uwekezaji katika utoaji wa huduma za maji. Taratibu na mifumo ya utoaji wa mikopo hiyo zitaainishwa kama ilivyoelekezwa katika miongozo ya maombi ya mikopo inayotolewa na Waziri.
2.0 Matumizi ya Fedha
Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira na Kanuni za Mfuko wa Taifa wa Maji, matumizi ya fedha yatakuwa kama ifuatavyo:
-
Si chini ya asilimia themanini na nane (88%) ya fedha zote zinazowekwa katika Mfuko zitatumika kwa gharama za uwekezaji wa mtaji katika miradi ya maji;
-
Si zaidi ya asilimia kumi (10%) ya fedha zinazowekwa katika Mfuko zitatumika kwa gharama za kiutawala na uendeshaji zinazohusiana na maendeleo ya maji, ikijumuisha maandalizi ya miradi, usanifu, usimamizi, ufuatiliaji na tathmini, pamoja na ufuatiliaji unaofanywa na Wizara na RUWASA kwa uwiano wa asilimia 60% na 40% mtawalia; na
-
Si zaidi ya asilimia mbili (2%) ya fedha zinazowekwa katika Mfuko zitatumika kwa gharama za uendeshaji wa Mfuko.
3.0 Uteuzi wa Miradi ya Maji
Sura hii inafafanua aina na vigezo vya uteuzi wa miradi ya maji inayostahili kufadhiliwa na Mfuko wa Taifa wa Maji. Neno mradi wa maji linafafanuliwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira kumaanisha mradi wa ujenzi, upanuzi au ukarabati wa miundombinu ya huduma za maji na usafi wa mazingira pamoja na uendelezaji, ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za maji.
Aidha, Kanuni ya 5 ya Kanuni za Mfuko wa Taifa wa Maji za mwaka 2019 inaainisha kuwa miradi ya maji itakayotekelezwa kwa fedha za Mfuko inaweza kujumuisha miradi kutoka maeneo mapana yafuatayo:
-
Ulinzi na uhifadhi wa maeneo ya vyanzo vya maji;
-
Uendelezaji wa miundombinu ya hifadhi ya maji, usalama na ulinzi wa rasilimali za maji; na
-
Ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya huduma za maji na usafi wa mazingira.
Miradi ya maji inayostahili kufadhiliwa itatokana na maeneo makuu mawili ya sekta, ambayo ni Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira (ujenzi, upanuzi au ukarabati wa miundombinu ya huduma za maji na usafi wa mazingira) na Usimamizi wa Rasilimali za Maji (Miradi ya Usimamizi wa Maeneo ya Vyanzo vya Maji – CMPs).
3.1 Miradi ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira
Kwa madhumuni ya kupata fedha kutoka Mfuko wa Taifa wa Maji, mradi wa huduma za maji na usafi wa mazingira unamaanisha miradi ya ujenzi, upanuzi au ukarabati wa miundombinu ya huduma za maji na usafi wa mazingira. Miradi hiyo inaweza kutekelezwa na Wakala wa Utekelezaji (IAs) ama kwa kutumia wakandarasi au kwa njia ya force account.
3.2 Miradi ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Inayostahili
Miradi ya huduma za maji na usafi wa mazingira itakayofadhiliwa na Mfuko wa Taifa wa Maji itahusisha miradi ya ujenzi, upanuzi au ukarabati wa miundombinu ya huduma za maji na usafi wa mazingira kama ifuatavyo:
(i) Ujenzi wa Mradi wa Maji unamaanisha uanzishaji wa miundombinu mipya ya huduma za maji na usafi wa mazingira, ikijumuisha vyanzo vya maji, maeneo ya kuchotea maji, miundombinu ya usafirishaji wa maji, vituo vya hifadhi ya maji au mitandao ya usambazaji wa maji.
(ii) Upanuzi wa Mradi wa Maji unamaanisha kuongeza au kupanua miundombinu iliyopo ya huduma za maji na usafi wa mazingira, ikijumuisha vyanzo vya maji, maeneo ya kuchotea maji, miundombinu ya usafirishaji wa maji, vituo vya hifadhi ya maji au mitandao ya usambazaji wa maji.
(iii) Ukarabati wa Mradi wa Maji unamaanisha kurejesha au kujenga upya miundombinu ya huduma za maji na usafi wa mazingira, ikijumuisha vyanzo vya maji, maeneo ya kuchotea maji, miundombinu ya usafirishaji wa maji, vituo vya hifadhi ya maji au mitandao ya usambazaji wa maji.