Huduma za Mikopo

Kulingana na Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) unatakiwa kusaidia uwekezaji katika miradi ya maji kwa njia ya ruzuku au mikopo.

Mikopo ya NWF yenye masharti nafuu inapatikana kwa mamlaka za maji na mashirika ya kijamii kwa ajili ya uwekezaji katika utoaji wa huduma za maji.

Taratibu na mifumo ya utoaji wa mikopo hiyo itafuatwa kama ilivyoainishwa katika miongozo ya maombi ya mikopo iliyotolewa na Waziri.

Miradi ya maji inayostahili kufadhiliwa na Mfuko itachaguliwa kwa kuzingatia vigezo vilivyobainishwa chini ya Miongozo hii.

Kanuni ya 6 ya Kanuni za Mfuko wa Taifa wa Maji inaainisha taratibu zinazopaswa kuzingatiwa katika uteuzi wa miradi ya maji kwa ajili ya ufadhili wa NWF. Taratibu hizi zitafuatwa kwa mujibu wa miongozo ya bajeti iliyowekwa chini ya Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015. Taratibu hizo ni kama ifuatavyo:

Hatua ya 1: Utambuzi na uandaaji wa mapendekezo ya miradi na Wakala wa Utekelezaji (IAs) kwa mujibu wa Mwongozo wa Usanifu wa Sekta ya Maji uliosasaishwa;

Hatua ya 2: Uwasilishaji wa mapendekezo ya miradi ya maji na Wakala wa Utekelezaji kwa Wizara kwa ajili ya uhakiki;

Hatua ya 3: Uwasilishaji wa orodha ya miradi ya maji kutoka Wizara kwenda kwa Mfuko kwa ajili ya tathmini na uchambuzi wa awali;

Hatua ya 4: Tathmini na uchambuzi wa awali wa orodha ya miradi iliyowasilishwa na Mfuko na kutoa mapendekezo kwa Waziri;

Hatua ya 5: Kuzingatia na kuidhinisha na Waziri orodha ya miradi ya maji iliyopendekezwa na NWF;

Hatua ya 6: Kuwasilisha miradi ya maji iliyochaguliwa Bungeni kwa ajili ya kutengewa bajeti; na

Hatua ya 7: Utekelezaji wa miradi ya maji iliyoidhinishwa.