Biography & Profile
Inj. ABDALLAH A. M. MKUFUNZI
Eng. Abdallah A. M. Mkufunzi ni Mhandisi Mtaalamu wa Mitambo mwenye uzoefu mkubwa wa zaidi ya miongo minne katika sekta ya rasilimali za maji na miundombinu nchini Tanzania. Ana Shahada ya Uhandisi wa Mitambo kutoka Chuo Kikuu cha Bangalore, India, na Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Pamoja wa Rasilimali za Maji kutoka Chuo Kikuu cha Cairo, Misri, na ni Mhandisi Mtaalamu aliyesajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).
Katika taaluma yake iliyotukuka, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu za uongozi na kitaalamu ndani ya Wizara ya Maji na taasisi zake, ikiwemo kuhudumu kama Kaimu Mtendaji Mkuu na baadaye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF). Utaalamu wake unahusisha Usambazaji wa Maji Mijini na Vijijini, Usafi na Mazingira, Upangaji na Utekelezaji na Miradi, Ufuatiliaji wa Kibiashara na Utendaji wa Mamlaka za Maji, Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa, Pamoja na Mifumo ya Mitambo kwa Miradi Mikubwa ya Miundombinu.
Eng. Mkufunzi amechangia kwa kiasi kikubwa katika mipango mikuu ya kitaifa ikiwemo Uanzishwaji wa Mamlaka za Maji na Majitaka, ukarabati wa vifaa vya kuchimba Visima na Mitambo, ujenzi wa Miundombinu ya kimkakati ya Maji, na utekelezaji wa Mifumo ya Usimamizi wa Utendaji ndani ya Taasisi za Serikali.
Aidha, ametoa mchango muhimu katika uandaaji wa sera, tafiti za upembuzi yakinifu, Maandalizi na Tathmini ya zabuni, pamoja na kujenga uwezo kupitia Mafunzo, Uanagenzi na ushiriki katika Makongamano ya kitaifa na kimataifa. Akitambuliwa kwa umahiri wake wa kitaalamu, uongozi madhubuti na kujitolea kwa huduma ya umma, Eng. Mkufunzi anaendelea kuchangia maendeleo endelevu ya rasilimali za maji na usimamizi wa miundombinu nchini Tanzania.