Biography & Profile
Leonard Vincent Challe ni Mtaalamu wa Fedha na Uhasibu, aliyezaliwa tarehe 28 Januari 1977 jijini Dodoma. Ana Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uhasibu na Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe (2011) na ni Associate Certified Public Accountant (ACPA) tangu Mei 2012. Aidha, ana Stashahada ya Juu katika Uhasibu (Advanced Diploma in Accountancy) kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM). Ana uzoefu mkubwa katika usimamizi wa miradi inayofadhiliwa na wahisani, usimamizi wa mali, uchambuzi wa hatari, ukaguzi wa kodi, Maandalizi ya Bajeti na taarifa za fedha, pamoja na utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya uhasibu (IPSAS na IFRS).
Kitaaluma, Bw. Challe kwa sasa anahudumu kama Mkurugenzi wa Fedha na Uhasibu katika Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) tangu Februari 2025. Kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi wa Fedha na Uhasibu pamoja na Meneja wa Fedha na Utawala katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), ambapo alisimamia sera za fedha, udhibiti wa bajeti, ukaguzi wa ndani na nje, pamoja na usimamizi wa rasilimali watu.