Biography & Profile
James M. Kalimanzila ni Mtanzania aliyezaliwa tarehe 5 Mei 1988 katika Kijiji cha Iyenze, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Ni mtaalamu wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, akiwa na Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Rasilimali Watu (MSc. Human Resource Development) kutoka Chuo Kikuu cha Airlangga, Indonesia, pamoja na Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma.
Kwa sasa, Bw. Kalimanzila anahudumu kama Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi (Director of Corporate Services) katika Mfuko wa Taifa wa Maji (National Water Fund – NWF) makao makuu Dodoma. Katika nafasi hii, anasimamia uratibu wa maandalizi na utekelezaji wa programu na miradi ya NWF, uundaji na utekelezaji wa sera na taratibu za ndani, upangaji na usimamizi wa bajeti, ufuatiliaji na tathmini ya utendaji, pamoja na masuala ya kibunge kwa kushirikiana na Wizara Mama.
Kabla ya kujiunga na NWF, Bw. Kalimanzila alihudumu katika Wizara ya Maji kama Afisa Rasilimali Watu Daraja la II na baadaye Daraja la I, akisimamia mipango ya rasilimali watu, ajira, mafunzo, kupandishwa vyeo, masuala ya mafao ya kustaafu, na tafsiri ya sheria na kanuni za utumishi wa umma. Pia amewahi kupewa majukumu ya ziada yakiwemo kuwa Afisa Bajeti, Mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA), na Katibu Mkuu wa Klabu ya Michezo ya Maji. Ni kiongozi mwenye uzoefu, nidhamu, na maono ya kuimarisha ufanisi na uwajibikaji katika taasisi za umma.